Shirika letu, Empowering Churches Mission (ECM), huwezesha makanisa yaliyoko maeneo mbalimbali ya ulimwengu yenye umasikini uliokithiri, kujikwamua na umasikini huo katika kufanya kazi ya Mungu ya kuendeleza na kutimiza Agizo Kuu la Bwana wetu Yesu Kristo la kuhubiri Injili (Mathayo 28:19-20), kuanzia na Afrika tulipo. Hufanya hivyo kupitia Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) kwa kuzitumia kama njia ya kuhimiza ushirikiano kati ya makanisa ya eneo husika, kuyawezesha kufanya vitu kwa urahisi, kwa uwezo zaidi na kwa haraka zaidi, kupitia kushirikiana kwa wao kwa wao. Makanisa hufanya hivyo kwa kuchangia rasilimali. Hatimaye, huwa na nguvu zaidi na uwezo zaidi wa kufanya vitu ambavyo, vinginevyo, yasingeweza kuvifanya kama kila kanisa lingebaki peke yake au vingechukua muda mrefu kuvifanikisha. Kupitia ushirikiano wa namna hiyo, makanisa hata yanaweza kuanzisha shughuli za kibiashara zielekeazo kuwa na faida, kujiingizia kipato, kujinasua kutoka utegemezi mmoja tu wa makusanyo ya kanisani wakati wa ibada, ambayo huwa madogo sana kukidhi mahitaji ya uhai na maendeleo ya makanisa. Neema hiyo ya makanisa kuwa na biashara za kuingiza kipato pia huwa na matokeo yanufaishayo jamii iyazungukayo kwa kuajiriwa nayo. Kwakuwa sehemu kubwa ya Wakristo wa makanisa hayo hutokana na jamii izungukayo makanisa hayo, nao unufaika na shughuli hizo za makanisa, kwa kuajiriwa nayo. Ikizingatiwa kwamba jamii nyingi barani Afrika, ikiwemo hata baadhi ya sehemu nyingine za ulimwengu ni masikini kupindukia, upatikanaji wa shughuli za kuingiza kipato kwenye makanisa husika, pia huinua hali ya maisha ya jamii inayoyazunguka kupitia ari waipatayo Wakristo wa makanisa hayo na jamii vijijini, ikiwemo hata watu mmoja mmoja, wakiiga vitega uchumi wavionavyo makanisani. Pia huinua uwezo wa Wakristo wa makanisa hayo kuweza kumtolea Mungu katika kazi yake kupitia makanisa yao, kuliko hapo awali.
Kwa kuwa ni utashi na ucha Mungu wa viongozi wa makanisa kushirikiana, kama hatua ya makusudi ya kutii Bwana wetu Yesu Kristo kupendana wenyewe kwa wenyewe (Yohana 13:34-35) na kumtumikia ipasavyo (Yohana 17:11, 21), ni jambo liwezekanalo ili makanisa yafanikiwe kuendeleza Agizo Kuu la Bwana wetu Yesu Kristo (Mathayo 28:19-20).
Pia, kwakuwa Mungu yupo pamoja nasi daima kutuwezesha Wakristo waliozaliwa mara ya pili, yakiwemo makanisa yao, kufanya vitu ambavyo vinginevyo haviwezekani, ushirikiano kati ya makanisa kupitia Kamati za Maeneo za Uwezeshaji, ni njia ya kuondoa hofu ambayo shetani aliweka katika akili ya viongozi wa makanisa kwa kuteka fikira yao ili wajione na kuendelea kujiona kutokuwa na uwezo wowote kwasababu ya kutokuwa na pesa mkononi au kwenye akaunti zao za benki.
Ili makanisa yajiunge kuwa wanachama wa kamati ya eneo husika, kila kanisa hulipa ada fulani ndogo iliyowekwa na kamati ya eneo husika kama kiingilio, kulingana na hali ya maisha ya eneo hilo. Kwahiyo, ada ipokelewayo na Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM), hubaki nayo kama pato la kusaidia kamati husika kuendesha shughuli zake, kulingana na Mipango Mkakati yake ya miaka kadhaa mbele, Mipango ya Kazi ya Mwaka na Bajeti za Mwaka ya Makanisa ya Eneo husika, itunzwayo na Waweka Hazina wa kamati husika.
Wachungaji ambao makanisa yao yanaendeshwa na kuongozwa kwa msingi wa Biblia, yaliyoko vijijini kwenye makazi ya watu, kwenye kila eneo la mraba wa kilometa nne (4) na yaliyoko mijini kwenye eneo la mraba wa robo (¼ ) kilometa, ambalo pia ni makazi ya watu, ndio huunda Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM), kuhakikisha kwamba makanisa yao yanawezeshwa kiuchumi ipaswavyo, kuweza kutekeleza ipasavyo Agizo Kuu la Bwana wetu Yesu Kristo la kuhubiri Injili (Mathayo 28:19-20). Kwahiyo, Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) zinapaswa kuwa kila mahali ambapo makanisa ambayo msingi wake ni Biblia yapo, kama njia ya kuyaleta pamoja, kushirikiana katika kuhakikisha maendeleo ya makanisa ya eneo yanakuwepo, kuanzia na kushirikiana kujisaidia yenyewe kwa yenyewe, yakitumia uwezo yalio nao. Pia kama njia ya shirika letu Empowering Churches Mission (ECM), kupitisha msaada kwa makanisa ya eneo kadiri ilivyopendekezwa na Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) kwa vitu vilivyo nje ya uwezo wake. Katika kufanya hivyo, Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM), zinakuwa njia ya kuwezesha makanisa, kadiri ya mahitaji yake yanavyoibuliwa na mapendekezo yanayofanywa na kamati, kwa kutumia mfumo huanziao shinani mwa eneo husika kwenda juu. Pia ni njia ya kuinua na kuhamasisha upendo na ushirikiano kati ya makanisa ya eneo moja kufanya kazi kwa kushirikiana katika kuimarisha kazi ya Mungu kwenye eneo husika. Vilevile ni njia ya kuoneshana na kuhakikishiana upendo wa Kristo kati ya makanisa (Yohana 13:34-35).
Kwahiyo, Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) zisingoje kuundwa. Ziundwe kila mahali ulimwenguni, mara zipatapo taarifa hii au zijuapo hivyo, hata kabla Empowering Churches Mission haijasajiliwa katika nchi hizo. Hii ni kwasababu Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) ni njia ya kuwezesha makanisa katika vijiji na mitaa mbalimbali ya maeneo husika na kuhakikisha kwamba Ukristo unakuwa na nguvu na kuzidi kuwa na nguvu, kuuokoa ulimwengu kutoharibiwa na shetani.
Pia kwahiyo, makanisa katika mitaa ya maeneo mbalimbali ya ulimwengu yanahamasishwa na kuombwa kuunda kamati hizo mara yajuapo hivyo kutokana na ukurasa huu wa Kwasababu upendo wa Kikristo haupaswi kungoja kuoneshwa hadi shirika lisajiliwe katika nchi husika. Ni jukumu la Kibiblia lipaswalo kuoneshwa na kuwepo wakati wote. Kwa jinsi vile Neno la Mungu lipaswavyo kuhubiriwa wakati wote, ndivyo Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) zipaswavyo kuundwa na kufanya kazi wakati wote kwa utukufu wa Mungu.
Vilevile kwa kuwa kupendana ni amri kutoka kwa Mungu (Yohana 13:34-35), Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) zinapaswa kuundwa kila mahali makanisa yapo, kuhakikisha uwepo upendo wa Mungu kati yake wakati wote. Hii ni kwasababu jukumu la kupendana si mradi au mpango upaswao kungoja kuanza tarehe fulani. Unapaswa kuwepo daima. Ambapo haupo, ni ukosefu wa utii kwa Mungu, ujulikanao kuwa dhambi. Kwahiyo, Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) yapasa ziundwe na kuhakikisha zimekuwa zana na njia ya kuhakikisha ushirikiano na upendo kati ya makanisa.
Uundaji wake katika eneo lolote pia ushawishi makanisa katika maeneo ya jirani na ng’ambo yake, nayo kufanya hivyo na hatimaye kuwa suala lifanyikalo kitaifa katika nchi nzima husika. Kwahiyo, Empowering Churches Mission inahimiza viongozi wa makanisa katika kila eneo husika ulimwenguni, kuunda Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) bila kukawia na kuhakikisha zinafanya kazi ipasavyo kama namna ya kudhihirisha utashi wao kushirikiana na kupendana, kuchangia kuuwezesha mwili wa Kristo kuwa na nguvu na kuongezeka nguvu kuliko tofauti na hivyo.
Makanisa ambayo msingi wake ni Biblia ni yale ambayo imani yake, mahubiri yake na mafundisho yake yanaemegea tu Neno la Mungu kama lilivyo ndani ya Biblia, bila kuongeza chochote au kubadilisha au kuchakachua na vitu vya Imani potofu. Kwahiyo, wanachama wa Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) wanao uwezo kubaini makanisa kama hayo kwasababu ya kuwa wenyeji wa eneo husika.
Kiuhalisia, Kamati za Eneo za Uwezeshaji Makanisa zinapaswa kuundwa na Wachungaji wa makanisa yaliyo hai ambayo msingi wake ni Biblia wa kila eneo husika, baada ya mmojawapo wa Wachungaji ametembelea tovuti ya Empowering Churches Mission, akasoma na kuelewa yaliyomo. Ndipo aitishe mkutano wa Wachungaji wa Makanisa ambayo msingi wake ni Biblia, kuunda kamati baada ya yeye mwenyewe kuwa ameelewa vizuri na kujihami na maelezo. Mkutano yapasa utangazwe vizuri kwa Wachungaji wote wa Makanisa ya eneo ambayo msingi wake ni Biblia ili waweze kuujua, ikiwemo mahali, tarehe na wakati utakapofanyika, hususani Jumapili mchana baada ya ibaada za asubuhi au siku na wakati mwingine unaofaa.
Mikutano kama hiyo ya uundaji kamati, yapasa ihudhuriwe na Wachungaji wawakilishao makanisa katika eneo, ambao si chini ya idadi ya nusu ya makanisa katika eneo ambayo msingi wake ni Biblia. Pia kila kamati itabidi iwachague baadhi ya Wachungaji waliohudhuria mkutano kuwa viongozi. Viongozi hao watakuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina na Washauri wasiopungua watatu na wasiozidi tisa.
Mwenyekiti achaguliwe kwa msingi wa kuwa Mchungaji muadilifu na wa kuheshimiwa katika eneo, pia kuwa na uwezo wa kuongoza mikutano, ikiwemo kuwa na uwezo wa kuhamasisha na kuinua ushirikiano wa makanisa katika kufanya kazi ya Mungu kwenye eneo husika. Makamu Mwenyekiti naye itabidi awe na sifa zifananazo na za Mwenyekiti lakini hasa jukumu lake litakuwa ni kumsaidia Mwenyekiti katika shughuli zake, hasa atakapokuwa ameenda mahali kikazi au atakapomuomba kumsaidia au atakapokuwa afya yake si nzuri. Katibu pia naye itabidi kuwa Mchungaji muadilifu na mwenye kuheshimiwa katika eneo, mwenye uwezo wa kuandika muhutasari wa vikao katika lugha zalendo ya mahali pale au katika Kiingereza au Kifaransa, pia awe na uwezo wa kusambaza kwa wajumbe muhutasari wa kikao aliouandika, mnamo siku saba za kikao husika kumalizika, pia itabidi awe na uwezo wa kuitisha kikao kijacho katika wakati kwa kushauriana na Mwenyekiti. Katibu Msaidizi naye atakuwa na sifa zinazofanana na za Katibu lakini hasa atakuwa na jukumu la kumsaidia Katibu katika shughuli zake, hasa atakapokuwa ameenda mahali kikazi au atakapomuomba kumsaidia au atakapokuwa afya yake si nzuri. Mweka Hazina naye itabidi awe Mchungaji muadilifu na mwenye kuheshimiwa katika eneo. Zaidi ya yote, itabidi awe muaminifu hasa na masuala yahusianayo na pesa na mali nyingine. Pia itabidi awe na uwezo wa kuhakikisha kwamba kumbukumbu bora inatunzwa ya pesa zinazopokelewa na kulipwa pamoja na za mali nyingine husika za kamati au shirika, zilizopokelewa au zilizotolewa nje.
Itabidi kamati ikutane angalau mara moja kwa mwezi. Wakati yaibukapo masuala ya dharura ya kujadili na kufanyia maamuzi, kamati inaweza kukutana zaidi ya mara moja kwa mwezi mradi kikao husika kihudhuriwe na angalau nusu ya wajumbe.
Majukumu ya kamati ni haya yafuatayo:
(a) kubaini na kuweka kumbukumbu hai ya makanisa ya eneo husika ambayo msingi wake ni Biblia, kwa kuwafanya Wachungaji Viongozi wa makanisa ndani ya eneo, kila Mchungaji kujaza na kusaini Fomu maalumu ya Uanachama na kuiwasilisha kwa Katibu wa Kamati husika ya Eneo ya Uwezeshaji Makanisa, kwa ajili ya kuomba uanachama wa kanisa lake (Fomu hiyo inapatikana kwa kuipakua kutoka kiunganishi hiki: https://empowering-churches.org/wp-content/uploads/2024/08/Fomu-ya-Kuliombea-Kanisa-Kuwa-Mwanachama-wa-Kamati-ya-Eneo-ya-Uwezeshaji-Makanisa.pdf
(b) kushughulikia ipasavyo Maombi ya Makanisa kuwa wanachama na kukubali/kupokea baadhi ya makanisa ambayo msingi wake ni Biblia kuwa wanachama na kutokubali yale ambayo msingi wake siyo Biblia
(Maombi kama hayo yatashughulikiwa katika kikao maalumu na kukubali au kupokea makanisa yenye sifa stahiki kuwa wanachama (wa kamati) na kuyakataa (makanisa) yasiyo na sifa stahiki. Mwishoni mwa kikao, Katibu atasajili kwa kuorodhesha makanisa yaliyokubaliwa uanachama kwenye Daftari (Rejesta) ya Uanachama pia kuyapatia Kadi za Uanachama. Vilevile, atawatumia taarifa Wachungaji ambao maombi yao ya uanachama yalikataliwa. Wakati wa uanachama wa makanisa, Katibu pia ataondoa au kufuta kutoka kwenye Daftari au Rejesta ya Wanachama, makanisa ambayo Kamati ya Eneo ya Uwezeshaji Makanisa imesimamisha uanachama wake kwasababu ya utovu wa nidhamu au kwasababu ya kupokea ushahidi wa kuaminika wa kukiuka maandiko ya Biblia katika mahubiri au mafundisho yake ya Neno la Mungu licha ya imani yake kwenye machapisho kudai kuegemea kuwa msingi wa Biblia. Pia Katibu atafuta au kuondoa kwenye Daftari (Rejesta) ya Uanachama, makanisa yaliyojiuzulu uanachama au yaliyoacha au yaliyositisha huduma.)
(c) kuhamasisha/kuinua upendo na ushirikiano (Yohana 13:34 – 35, 1 Yohana 4:20) kati ya makanisa ya eneo katika kufanya kazi ya Mungu ya kuendeleza Agizo Kuu la Bwana wetu Yesu Kristo (Mathayo 28:19-20)
(d) kutumia Neno la Mungu ndani ya Biblia kuhamasisha makanisa ya eneo husika kuishi kwa amani kati yake na kujizuia kufanyiana uhasama
(e) kuwa njia ya makanisa ya eneo kuwa na mpango au agenda moja ya kufanikisha kumtumikia na kumwakilisha Yesu Kristo katika eneo, kama ngome au nguvu moja ili katika kufanya hivyo, makanisa yamiliki na kuendeleza kwa pamoja mahitaji ya maendeleo ya huduma, ikiwemo pia mahitaji ya maendeleo ya jamii kwa ujumla, pamoja na mambo mengine, kubadili mtazamo wao ipasavyo, wakaanza kuona Wakristo wanachama ndani ya makanisa yao, wasio na ulemavu au upungufu wowote, kama mali na vifaa maalum vya maendeleo, wakavitumia kama mtaji wao wa kwanza katika kuwawezesha kuanzisha vitega uchumi kuliko kutofanya hivyo kwasababu ya kujiona kutokuwa na mtaji wowote kwahiyo kutoweza kuanzisha na kujishughulisha katika biashara yoyote
(f) kukubali namna ya makanisa kwenye eneo ambayo msingi wake ni Biblia yatashirikiana kusaidiana katika kufanya kazi ya Mungu, ikiwemo kanuni na maadili yatakayofuata na mambo yatakayopaswa kujizuia kuyafanya
(g) kubaini mahali kwenye eneo la kamati ambapo kunakosekana makanisa yaendeshwayo kwa msingi wa Biblia na kuyapanda (kuyaanzisha)
(h) kuwa njia ya Empowering Churches Mission kufanya upenguzi wa eneo (baseline survey) ili kulijua vizuri, ikiwemo kufanya utafiti wa kujua mambo yapasayo kufanywa kuwezesha miradi husika kufanikiwa (feasibility studies) na mipango ya biashara (business plans) kwa ajili ya biashara mbalimbali, kubaini viwezekanavyo kufanikiwa endapo vitaanzishwa na makanisa mbalimbali ya eneo, ikiwemo baadhi yake kushirikiana pamoja
(i) kila kamati kuandaa, kufuata na kufanya marejeo yake kila mwaka Mpango Mkakati wake wa miaka mitatu au zaidi
(j) kila kamati kuandaa Mpango wake wa Kazi wa Mwaka kabla ya Januari ya mwaka husika na kuhakikisha kwamba inautumia na kuufanyia marejeo wakati wowote inapobidi, kuendana na mabadiliko ya mambo katika eneo au katika nchi kwa ujumla
(k) kila kamati kuandaa na kutumia Bajeti yake ya Mwaka kabla ya Januari ya mwaka husika na kuhakikisha inaufanyia marejeo wakati wowote inapobidi, kuendana na mabadiliko ya mambo katika eneo au katika nchi kwa ujumla
(l) kuhimiza makanisa moja moja ya eneo kutumia uwezo yalio nao kuanzisha, kila moja peke yake au kwa kushirikiana, vitega uchumi kwa njia ya kujitegemea, hususani kujenga majengo na kuendesha shule, vyuo, hospitali, vituo vya afya, nyumba za wageni, migahawa, hoteli, vituo vya mikutano kwa ajili ya kukodesha wateja, nakadhalika
(m) kuhimiza makanisa moja moja kupendekeza vitega uchumi yafikiriayo vinawezekana kufanikiwa katika maeneo yake lakini yafikiriayo kuwa nje ya uwezo wake, kuanzisha kwa njia ya kujitegemea yenyewe ili yawasilishe mapendekezo hayo kwa kamati (ya eneo), iyawasilishe kwa Empowering Churches Mission kwa ajili ya uwezekano ya kuyasaidia hasa katika masuala ya kuyafanyia utafiti wa kujua nini kifanyike kuwezesha biashara na miradi husika kufanikiwa (business plans and feasibility studies)
(n) kusaidia kanisa moja moja kuanzisha vitega uchumi kwa kuyaunga mkono na kuyaunganisha na ngazi ifuatayo na viongozi wa ngazi ifuatayo ya Empowering Churches Mission ili iyasaidie ipasavyo kuanzisha vitega uchumi viashiriavyo kufanikiwa
(o) kuwa njia ya kuwa wenyeji wa kuendesha mafunzo tosha ya viongozi wa makanisa wa eneo katika masuala ya stadi za maisha, ujasiriamali, biashara, menejimenti, usimamizi bora wa miradi na mbinu za kunadi biashara
(p) kubaini Wachungaji, viongozi wengine wa makanisa na Wakristo kwa ujumla katika eneo, ambao wana haja ya kujifunza Theolojia na Mafunzo ya Biblia au wapungukiwao hayo mafunzo na kuwasaidia kufanya hivyo, ikiwemo wahitajio kusoma masomo ya Chuo Kikuu katika masomo hayo
(q) kubaini majengo ya makanisa ambayo msingi wake ni Biblia kwenye eneo la kamati hiyo, yastahiliyo au yahitajiyo ukarabati wa haraka kidharura na kuhamasisha ushirikiano wa makanisa mengine katika eneo, ambayo msingi wake ni Biblia, kuyawezesha makanisa hayo yenye uhitaji wa kukarabatiwa, kila kanisa kufanya hivyo kadiri ya idadi ya Wakristo wake ambao ni watu wazima, wasio na ulemavu
(r) kubaini majengo ya makanisa ambayo msingi wake ni Biblia, yaliyo kwenye hatua ya kujengwa na kuhamasisha ushirikiano wa makanisa ya eneo ambayo msingi wake ni Biblia kuyasaidia kujenga kadiri ya idadi ya Wakristo wake ambao ni watu wazima, wasio na ulemavu
(s) kuteua benki pa kufungua akaunti kwa ajili ya kamati ya eneo husika, ili Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi na Mweka Hazina ndio wafungue akaunti hiyo na kuiendesha
(t) kuhamasisha makanisa ya eneo ambayo msingi wake ni Biblia, kutumia fursa ya uwepo wa idadi ya Wakristo wake kuanzisha na kuendesha Benki za Jamii za Vijijini (Village Community Banks), kwa kifupi zijulikanazo kama VICOBA au kuanzisha na kuendesha vyama vya ushirika vya akiba na kukopa (Savings and Credit Cooperative Societies) kwa kifupi vijulikanavyo kama SACCOS.
(v) kuwa njia ya Empowering Churches Mission kuhimiza makanisa ambayo msingi wake ni Biblia katika maeneo ya vijijini, ambapo kamati inawajibika, kumiliki, kuanzisha na kuendesha mashamba yaelekeayo kufanikiwa kibiashara ya kiasi cha upana wa kati na kubwa, yaanziayo hekitari 50 hadi 100 na zaidi, kwa kutumia materekita ya kukodi kutoka kwa wenyewe au yaliyonunuliwa kwa mkopo na kamati au kanisa mojawapo katika eneo, kutoka kwa benki ziyakopeshazo, kuyawezesha makanisa kuyatumia kulima mazao mbalimbali stahiki, wakati wa msimu wa kilimo, yenye muelekeo wa kuleta faida kupitia mapato ya msimu, baada ya mavuno, ili yajikomboe kutokana na umasikini wa kipato, pia kuwa mfano wa maendeleo ya kiuchumi wa kuigwa katika jamii inayoyazunguka
(w) kuwa njia ya Empowering Churches Mission kuhimiza makanisa ambayo msingi wake ni Biblia katika maeneo ya mjini ambapo kamati inawajibika, kumiliki, kuanzisha na kuendesha biashara ielekeayo kufanikiwa, kuyawezesha kuitumia kuingiza kipato endelevu ili yajikwamue kutoka umasikini wa kipato, pia kuwa mfano wa maendeleo ya kiuchumi wa kuigwa katika jamii inayoyazunguka
(x) kuhimiza makanisa katika eneo ambayo msingi wake ni Biblia kuwezeshana, kwa kutegemea uwezo binafsi yalio nao, wakati pia yategemeapo msaada wowote uwezekanao wa Empowering Churches Mission, kuliko tu msaada wa kutoka, ambao wakati mwingine unaweza kuchukua muda muda mrefu kwasababu ya makanisa mengine katika eneo, ambayo msingi wake ni Biblia kuutegemea pia
(y) kuwa njia ya kufunza lugha ya Kiingereza kwa viongozi wa makanisa wa eneo wasioijua, kuijua kwa ajili ya kuitumia katika kuhubiri Injili ya Yesu Kristo kimataifa au wakati wa kuwa wenyeji wa wahubiri na walimu wa Neno la Mungu wa kimataifa kwenye makanisa yao na katika eneo kwa ujumla
(z) kuwa njia ya kuhimiza makanisa ya eneo kuhakikisha kwamba Wakristo wote ndani ya makanisa hayo wanajua kuandika na kusoma, kuweza kusoma na kuandika vizuri, ikiwemo kusoma vizuri Biblia na kujua Hisabati za Msingi, kuwawezesha kuanzisha na kuendesha vizuri shughuli za kuijiingizia kipato
Kwakuwa, pamoja na mambo mengine, Kamati za Maeneo za Uwezeshaji Makanisa (KMUM) ni njia ya kuhakikisha utii kwa Mungu unahamasishwa, pia kwamba kwa namna hiyo nguvu na uwezo stahiki vipo kwa ajili ya kushamirisha Ufalme wa Mungu katika eneo, zinapaswa kuundwa na kuhakikishwa zinafanya kazi mahali popote yalipo makanisa ambayo msingi wake ni Biblia. Kwahiyo, mahali popote kamati hizo zipo na kufanya kazi vizuri, ni ushuhuda kwamba makanisa husika yanashirikiana yapasavyo kufanikisha Agizo Kuu la Bwana wetu Yesu Kristo la kuhubiri Injili (Mathayo 28:19 -20) katika eneo, ili kuwa jeshi la kiroho lenye nguvu katika eneo.